CATTLE
Dume
Mzuri Kwa Uzalishaji Wa Ng’ombe Wa Maziwa
Tunaangalia uchaguzi
wa dume mzuri kwa uzalishaji wa ng’ombe wa maziwa, pamoja na aina ya malisho
ambayo mfugaji anaweza kuyatumia kuweza kukabiliana na changamoto ya malisho
kwa ng’ombe.
Wafugaji wengi wamekuwa wakipata ng’ombe wanaozalisha kidogo na
kwa kiwango cha chini kutokana na kuangalia ukubwa wa gharama ya mbegu
wakidhania kuwa ndiyo upatikanaji wa ng’ombe bora. Vinasaba husaidia kwa
kiwango kikubwa katika kupata ng’ombe mzuri wa maziwa.
Kuwepo kwa ongezeko la uzalishaji wa maziwa hutegemeana na vitu
viwili ambavyo ni kuboresha mifugo kwa kufanya uchaguzi sahihi wa kizazi pamoja
na usimamizi mzuri unaojumuisha lishe kamili, malazi mazuri, upatikanaji wa
maji,kuwa karibu na wanyama pamoja na utoaji wa kinga na tiba dhidi ya
magonjwa.
Vinasaba pamoja na usimamizi mzuri ni vitu viwili
vinavyotegemeana. Bila kuwa na uzao mzuri, uzalishaji wa wanyama pamoja na
usimamizi utakuwa wa hali ya chini sana, na bila usimamizi mzuri wanyama bora
hawawezi kuonesha ubora wao katika uzalishaji.
Uzao mzuri humpa nafasi kubwa mfugaji kutambua sifa na
uzalishaji utakaopatikana katika uzao ujao. Endapo mfugaji atafanya uchaguzi
mbaya basi ni hakika atakuwa na uzalishaji hafifu wa maziwa, kuzorota kwa afya
ya mnyama pamoja na maisha mafupi.
Muda wa kufanya tafiti
Wafugaji wengi wamekuwa wakifikiria mbegu pale tu ng’ombe
anapokuwa tayari anahitaji kupandwa na matokeo yake ni kuwa, kutokana na haraka
ya kutaka kumhudumia ng’ombe huyo, basi mfugaji atakuwa tayari kuchukua mbegu
yoyote ile atakoyopatiwa na wataalamu. Kwa mantiki hiyo, hakuna muda
mfugaji atatumia kuchunguza aina ya dume aliyetumika kupatikana kwa mbegu hiyo
na badala yake, gharama hutumika kwa kiasi kikubwa kuonesha uwezo wa dume huyo.
Wafugaji wengi hufikiri kuwa kitendo cha mbegu kuuzwa kwa
gharama kubwa ni moja ya njia ya kutambua ubora wa dume. Wauzaji wengi wamekuwa
wakitumia njia hii kuwadanganya na kuwarubuni wafugaji.
Ni muhimu sana kwa mfugaji anaelenga kuzalisha maziwa kusoma na
kuelewa taarifa zote muhimu zilizotolewa kuhusu aina ya dume husika. Ili
kufanikiwa katika uzalishaji wa maziwa, ni muhimu kwa mfugaji kuwa makini na
kulichukulia kwa uzito suala la uchaguzi wa dume na kuelewa nini kinahitajika
bila kubahatisha. Mfugaji ni lazima atambue kuwa, dume huchangia asilimia 50 ya
kinasaba katika uzao wake hivyo ni muhimu sana kujua sifa za dume unayemchukua
kwa ajili ya uzalishaji. Pia ubora wa maziwa huchangiwa kwa kiasi kikubwa na
aina ya dume aliyetumika. Dume wa maziwa hutambulika kwa kuangalia kiwango cha
maziwa yanayozalishwa na ng’ombe aliyepandwa na dume huyo na mtamba aliyezaliwa
na ng’ombe huyo ambapo dume huyo husambaza sifa ya maziwa kutoka kwa ng’ombe
huyo hadi kwa mtamba.
Elewa maelekezo yaliyopo kwenye kabrasha la mbegu
Kielelezo cha vinasaba hutumika kupima uwezo wa mnyama kusambaza
vinasaba vyake kwenda kwa uzao ujao. Katalogi huwa na taarifa muhimu ambazo
zitamsaidia mfugaji kufanya uchaguzi mzuri wa dume ili kuwa na uhakika wa
kuendeleza kizazi baada ya kingine.
Tags:
NG'OMBE MAZIWA