Sasa


Faida za kufuga sungura

Faida za kufuga Sungura
HIZI NDIZO FAIDA ZA KUFUGA SUNGURA!


 Uzoefu wangu wa ukulima na ufugaji wa asili, sungura ni mnyama rahisi wa kufuga kwani hana gharama kubwa na ndiyo maana shughuli hii inaweza kufanywa na mkulima mdogo asiye na mtaji mkubwa, tena sungura akitunzwa vyema inavyostahili haugui kwa urahisi na pia lishe yake ni rahisi kupatikana.



Chakula cha sungura ni kama

  •  nyasi,
  • mboga kama vile sukuma, spinachi, kabichi, karoti, mchunga na
  •  pia waweza kununua chakula halisi cha sungura kutoka maduka ya vyakula vya wanyama.

Sungura akila vyakula hivi vibichi anakojoa mara kwa mara, na mkojo wake  unaweza kukuleta kipato kikubwa kwa sababu unatumika katika maabara.

Hata hivyo, kama unataka kumkinga na magonjwa ya tumbo, unashauriwa kukausha chakula chake, jambo ambalo pia husaidia asikojoe hovyo.

Nyama ya sungura ni tamu na inalingana na nyama ya kuku. Hii ni nyama nyeupe ambayo haina mafuta ya lehemu (cholesterol) na hiyvo wataalam wa lishe bora huhimiza matumizi ya nyama ya sungura kwani ni bora kwa afya.

Ufugaji wa sungura ni kitengo kidogo cha ustawi wa mifugo kwa minajili ya kuongeza uzalishaji wa nyama na pia kwa mapato.

Ingawa soko la nyama ya sungura haliko kwa wingi, lakini hilo lisikutishe mfugaji kwa sababu mara nyingi soko la bidhaa yoyote huwepo kutokana na kuwepo kwa bidhaa yenyewe. Yawezekana hulioni soko kwa sasa kwa sababu si wengi wanaofuga sungura, lakini pia ufugaji ukiongezeka soko lake ni kubwa.

Soko linaweza lisiwe kikwazo kikubwa ikiwa wajasiriamali wafugaji sungura wataunda umoja wao ambao utawasaidia kutafuta masoko.

Katika kipindi hiki ambacho Tanzania inashuhudia uwekezaji mkubwa katika mafuta na gesi pamoja na madini mbalimbali, ni dhahiri soko litakuwepo kwa sababu Wachina na watu kutoka mataifa mengine ni watumiaji wazuri wa nyama ya sungura.

Wakati inahimizwa kuhusisha bidhaa za ndani (local content) katika uwekezaji huo, ni vyema wanajamii kujikita katika miradi kama hii ya ufugaji wa sungura ili isitokee wawekezaji wa kigeni wakaagiza sungura wao kutoka ughaibuni kwa ajili ya kitoweo.

Ufugaji wa sungura ni biashara nzuri kwa sababu kwanza mafunzo yake tu kwa wakulima wanaotaka kufuga yanalipa, lakini bado unaweza kuuza sungura wako kwa wafugaji hao ukapata fedha. Sungura hai kwa ajili ya kufugwa anauzwa hadi TShs. 50,000 akiwa na uzito wa kilogramu 1.5 tu.

Lakini kwa vile sungura wanauzwa kulingana na uzito wao, ni muhimu sana kuwalisha vyema, lakini pia hiyo itawasaidia waweze kuzaliana na kumnufaisha mkulima.

Lazima mkulima anayefuga sungura kibiashara awe na mpango kazi mdogo wenye malengo yanayotekelezeka ili kuhakikisha kwamba daima anakuwa nao ili asipoteze soko lake.

Kuwa na sungura 100 na kuendelea kwa mwaka siyo kazi ngumu ukiwa umedhamiria na umejikita kwenye biashara hiyo.

Kama unafuga sungura jamii ya New Zealand White unaweza kunufaika pia na damu yake (rabbit serum) baada ya kuwachinja ambayo ina soko kubwa. Inaelezwa kwamba, damu ya sungura hao inakaribiana na damu ya binadamu na hivyo inahitajika sana kwa watafiti wa tiba. Katika nchi kama Marekani, galoni la lita 3 linauzwa kwa takriban Dola 15,000 (zaidi ya Shs. 30 milioni).

Lakini kuwemo katika orodha ya wauzaji wa damu ya sungura kwa ajili ya utafiti wa tiba inahitaji kazi kubwa. Unatakiwa uwe na sungura wa kutosha wa jamii hiyo na unatakiwa upate kibali maalum.

Sijajua kama utafiti wa aina hii unafanyika hapa Tanzania, lakini inawezekana haufanyiki kwa sababu zile zile kwamba hakuna wafugaji.

Usihesabu faida kwa kuangalia fedha utakazovuna kwa ufugaji wa sungura, bali angalia pia ni kiasi gani cha fedha unaokoa kwa kutokwenda buchani kununua nyama. Hizi ni fedha ambazo zinabakia mfukoni mwako na unaweza kuzihesabu kama ni faida.

Kwa kufuga sungura hulazimiki kuacha kazi yako ya kila siku, na hata kama unafuga kiasi tu, inakusaidia kupunguza gharama za matumizi ya nyumbani.

Kama ilivyo kwa biashara yoyote ile, huwezi kupata mafanikio kufumba na kufumbua. Unapaswa kutambua kwamba lazima uwe na mpango kazi. Lazima ujue kuwatunza sungura wako na kutafuta soko. Unapaswa pia kujua jinsi ya kupanga bajeti yako.

Kwa kufanya hivyo unaweza kuona faida, lakini inahitaji ustahimilivu na nidhamu ya hali ya juu kama ilivyo kwenye biashara yoyote.

Kwa mtazamo wangu mimi, lazima kuwe na idadi maalum ya kuzalisha sungura kwa mwaka ili uone faida.

Ili kuangalia gharama (vyakula, huduma, mahitaji na kadhalika) kwa biashara ya nyama ya sungura ili ilingane au iwe pungufu ya ile unayoitumia kununua nyama buchani, sungura jike mmoja anapaswa kuzaa wastani wa watoto 35 kwa mwaka.

Ili kufikia lengo hilo, sungura jike lazima lipandishwe kila siku 10 hadi 21 baada ya kuzaa na watoto wanaachishwa kunyonya baada ya kufikisha umri wa wiki nne. Hii maana yake atazaa mara 7 hadi 8 kwa mwaka. Kwa kutumia hesabu hiyo hapo juu, sungura jike, kama ni mbegu nzuri, atazaa watoto kati ya 50 hadi 60 kwa mwaka. Idadi ya watoto watakaokua itategemea mama yao ni mzuri kiasi gani katika unyonyeshaji na jitihada zako katika kuwatunza.

Sungura jike ambaye hawezi kufikia kiwango hicho cha uzazi lazima aondolewe. Kama sungura hazai, basi anakutia hasara kwa sababu anatumia chakula bila faida. Wastani wa uzito unaotakiwa ni kati ya kiloghramu 2 hadi 2.5 wakati sungura anapofikisha umri wa wiki nane hadi 10. Muda huo hutegemea pia na matunzo yako unayompatia, aina ya sungura, mazingira ya joto, na kiwango cha protini unachomchanganyia kwenye lishe yake.

Kama nilivyopata kusema, unaweza kuanza na mtaji mdogo, na siyo vibaya ukianza na wastani wa majike manne na dume moja, ukiwa na vifaa vya msingi. Ukiwa na kiwango hiki cha sungura, hata kama hutawauza kwa wafanyabiashara, familia itakuwa na uhakika wa lishe kwani unaweza kuchinja sungura wawili kwa wiki kwa mwaka mzima bila shida. 

Lakini unaweza kuuza nyama ya sungura kwenye maduka makubwa (super markets), mahoteli ya kitalii na kwa watu binafsi wanaohitaji nyama.

Jihadhari sana na madalali, kwa sababu wao wanapata faida sana kwa kununua sungura hai na kisha kuwauzwa kwenye migahawa kwa bei mbaya.

Mbolea inayotokana na kinyesi cha sungura ni nzuri sana kwa sababu haiwezi kuunguza mimea kama ilivyo kwa mbolea ya kuku. Kwa hyo unaweza kuitumia shambani kutengeneza kilimo hai kinachotakiwa.

Kama utamwaga kidogo chokaa kwenye banda la sungura kupunguza harufu ya kinyesi chao utaongeza ubora na thamani ya mbolea hiyo.

Bado ninatengeneza miundombinu katika shamba langu Yombo-Mwanadilatu, naamini nikikamilisha litakuwa shamba darasa kwa jamii yote. Karibuni sana

 Daima usikose kutembelea 
https://www.animalscience.care/


Previous Post Next Post