Sasa


Ulishaji sungura

Ulishaji wa Sungura

MATUNZO MUHIMU NA ULISHAJI WA SUNGURA WAKO

Kama mnyama yeyote sungura wanahitaji utunzaji  ili waweze kuzalisha kwa wingi.

Wanahitaji kujengewa chumba maalum  na kuangaliwa kila siku na kuhakikisha usafi wa vyumba hivi.
Na kama watoto wa binadamu, pia sungura wanahitaji kupewa chakula kisafi cha hali ya juu kilicho na madini ya protini na kalsiamu na pia kupewa maji safi.

Ikiwa mfugaji anataka kunufaika na sungura anaowafuga basi ni sharti ahakikishe wana afya njema, kwani hii ndiyo changamoto mojawapo kwa ufugaji wa sungura, magonjwa ya sungura hasa huwa ni ya tumbo na kifua. Tatizo hasa ni kwamba, wataalamu bado hawajagundua dawa maalumu za magonjwa ya sungura kwa hivyo ni muhimu kwa mfugaji kuhakikisha sungura wake hawapatwi na magonjwa.
Sungura aliye na afya ni yule ambaye
ü   ngozi yake ni nyororo,
ü  macho mazuri yasiyo na kasoro,
ü   asiye na vidonda vya ngozi, katika macho, midomo, au kwenye masikio.
Uchafu kwenye miguu na pua ni ishara ya ugonjwa wa kukohoa kwani sungura huosha pua zake kwa kutumia miguu ya mbele. Pia unaweza kumuweka chini na kutazama dalili za ugonjwa anaporuka.

Chakula cha sungura

Kama nilivyoeleza hapo awali, kila kizimba cha sungura lazima kiwe na eneo ama chombo cha kuwekea chakula, tena unaweza kuongeza chemba maalumu kwa ajili ya kuwekea nyasi.
Chemba hiyo ni vyema iwe na nyasi maalumu kila wakati – na wataalamu wa ufugaji sungura wanapendekeza majani aina ya Alfalfa, lakini kama unapata majani ya mchunga ni mazuri sana kwa sababu hawa jamaa wanayapenda mno kwani yana viinilishe vingi.
Sungura wanakula vyema nyasi zikiwa zimekatwa katwa katika kipimo cha inchi tatu au nne. Kusanya kitita cha majani na ukikate kwa panga kwa urefu huo.
Unaweza pia kumlisha sungura wako mikundekunde na jamii yake, kabichi, spinachi na Sukuma wiki. Usisahau kwamba wanakula pia mizizi na ikiwa karoti zinapatikana wapatie.
Hata hivyo, hakikisha unaondoa mabaki yote ya chakula ambacho wameshindwa kula. Ondoa kila siku kwenye kizimba na baada ya muda utagundua wanapendelea nini zaidi, kwa sababu unaweza usikute mabaki.
Walishe sungura wako mboga mboga kwa taratibu kama hawajazowea mpaka watakapokuwa wamezowea. Wakati mwingine wakil asana wanavimbiwa au hupata ugonjwa wa kuhara.
Pia uwalishe vyakula maalumu vya sungura vinanvyopatikana kwenye maduka ya vyakula vya mifugo. Unaweza kuwalisha hata njugu mawe kwa sababu wanazipenda pia.
Unaweza kupata mwongozo wa awali hata kwa mtu ambaye amekuuzia sungura hao namna anavyowalisha, lakini kama kuna ofisa ugani karibu yako, mtumie ili akuelekeze vyema.

Utunzaji wake
Achana na zile kauli za “Aisee, tazama wanavyopendeza”. Hawa ni mifugo, siyo wanyama wa mapambo na ni mifugo wazuri, wasafi zaidi na wasiopatwa na magonjwa ya mara kwa mara kama wanyama wengine.
Utagundua kwamba kila mnyama ana ghadhabu zake… wengine ni rahisi kuwahudumia, baadhi ni wagumu.
Unapomwinua sungura, mbebe kwa kumshika shingoni upande wa nyuma na weka mkono wako mwingine chini ya matako yake ili kuubalansi uzito. Kumwinua ovyo ni kumuumiza sungura na unaweza kumsababishia hata mikwaruzo na maumivu ya mifupa. Tena ni kinyume na haki za wanyama.
Miguu ndilo eneo ambalo sungura wa kufugwa huwa na matatizo ya kiafya.
Vidonda kwenye makanyagio vinaweza kutibiwa kwa kutumia pamba safi iliyochovywa kwenye dawa aina ya Campho–Phenique, ambayo hupatikana kwenye maduka ya dawa za mifugo. Matibabu ya muda yanaweza kuliondoa tatizo hilo.
Uvimbe unaweza kutibiwa kwa namna hiyo hiyo, lakini lazima uweke matandazo ya kutosha mahali wanapoishi ama uweke ubao ili wasikanyage kwenye waya wa kwenye kizimba.
Inzi na wadudu wengine warukao wanawasumbua sungura, na wanaweza kuzuiwa kwa kunyunyizia dawa za kuua wadudu ambazo zinapatikana kwenye maduka ya mifugo. Usitumie dawa za kupuliza kwa sababu zina madhara kwa sungura hasa katika mfumo wa upumuaji na zinaweza kuwaua.
Walishe sungura wako chakula maalumu kwa wastani wa wakia tatu kwa siku kwa kila mnyama. Wape maji safi na salama ya kutosha. Nyongeza ya chakula ni nyasi pamoja na majani mabichi au kabichi.
Pendelea vyakula vya nyongeza vya kijani. Kwa kuwa sungura wanacheua na mara nyingi hula usiku, basi hakikisha unawalisha vyema nyakati za jioni.
Kila kizimba lazima kiwe na jiwe la chumvi maalumu kwa sungura, ambalo linapatikana kwenye maduka ya vyakula vya mifugo. Hili ni muhimu kwa sababu linaongeza madini ya chumvi mwilini. Sungura daima hulilamba wakati wowote anapotaka. Bila kuweka madini ya kutosha kwenye milo yao, sungura jike anaweza kuwatafuna watoto wake.
Hakikisha vyombo unavyovitumia kulishia ni visafi daima, kuanzia vile vya chakula na maji.

Previous Post Next Post