MATUNZO MUHIMU NA ULISHAJI WA SUNGURA WAKO
Kama mnyama yeyote sungura wanahitaji utunzaji ili waweze kuzalisha kwa wingi.
Wanahitaji kujengewa chumba maalum na kuangaliwa kila siku na kuhakikisha usafi
wa vyumba hivi.
Na kama watoto wa binadamu, pia sungura
wanahitaji kupewa chakula kisafi cha hali ya juu kilicho na madini ya protini
na kalsiamu na pia kupewa maji safi.
Ikiwa mfugaji anataka kunufaika na
sungura anaowafuga basi ni sharti ahakikishe wana afya njema, kwani hii ndiyo
changamoto mojawapo kwa ufugaji wa sungura, magonjwa ya sungura hasa huwa ni ya
tumbo na kifua. Tatizo hasa ni kwamba, wataalamu bado hawajagundua dawa maalumu
za magonjwa ya sungura kwa hivyo ni muhimu kwa mfugaji kuhakikisha sungura wake
hawapatwi na magonjwa.
Sungura aliye na afya ni yule ambaye
ü ngozi yake ni nyororo,
ü macho mazuri
yasiyo na kasoro,
ü asiye na vidonda vya ngozi, katika macho,
midomo, au kwenye masikio.
Uchafu kwenye miguu na pua ni ishara
ya ugonjwa wa kukohoa kwani sungura huosha pua zake kwa kutumia miguu ya mbele.
Pia unaweza kumuweka chini na kutazama dalili za ugonjwa anaporuka.
Chakula cha sungura
Kama
nilivyoeleza hapo awali, kila kizimba cha sungura lazima kiwe na eneo ama
chombo cha kuwekea chakula, tena unaweza kuongeza chemba maalumu kwa ajili ya
kuwekea nyasi.
Chemba hiyo ni vyema iwe na nyasi
maalumu kila wakati – na wataalamu wa ufugaji sungura wanapendekeza majani aina
ya Alfalfa, lakini kama unapata majani ya mchunga ni mazuri sana kwa sababu
hawa jamaa wanayapenda mno kwani yana viinilishe vingi.
Sungura wanakula vyema nyasi zikiwa
zimekatwa katwa katika kipimo cha inchi tatu au nne. Kusanya kitita cha majani
na ukikate kwa panga kwa urefu huo.
Unaweza pia kumlisha sungura wako
mikundekunde na jamii yake, kabichi, spinachi na Sukuma wiki. Usisahau kwamba
wanakula pia mizizi na ikiwa karoti zinapatikana wapatie.
Hata hivyo, hakikisha unaondoa mabaki
yote ya chakula ambacho wameshindwa kula. Ondoa kila siku kwenye kizimba na
baada ya muda utagundua wanapendelea nini zaidi, kwa sababu unaweza usikute
mabaki.
Walishe sungura wako mboga mboga kwa
taratibu kama hawajazowea mpaka watakapokuwa wamezowea. Wakati mwingine wakil
asana wanavimbiwa au hupata ugonjwa wa kuhara.
Pia uwalishe vyakula maalumu vya
sungura vinanvyopatikana kwenye maduka ya vyakula vya mifugo. Unaweza kuwalisha
hata njugu mawe kwa sababu wanazipenda pia.
Unaweza kupata mwongozo wa awali hata
kwa mtu ambaye amekuuzia sungura hao namna anavyowalisha, lakini kama kuna
ofisa ugani karibu yako, mtumie ili akuelekeze vyema.
Utunzaji wake
Achana na zile kauli za “Aisee, tazama
wanavyopendeza”. Hawa ni mifugo, siyo wanyama wa mapambo na ni mifugo wazuri,
wasafi zaidi na wasiopatwa na magonjwa ya mara kwa mara kama wanyama wengine.
Utagundua kwamba kila mnyama ana
ghadhabu zake… wengine ni rahisi kuwahudumia, baadhi ni wagumu.
Unapomwinua sungura, mbebe kwa
kumshika shingoni upande wa nyuma na weka mkono wako mwingine chini ya matako
yake ili kuubalansi uzito. Kumwinua ovyo ni kumuumiza sungura na unaweza
kumsababishia hata mikwaruzo na maumivu ya mifupa. Tena ni kinyume na haki za
wanyama.
Miguu ndilo eneo ambalo sungura wa
kufugwa huwa na matatizo ya kiafya.
Vidonda kwenye makanyagio vinaweza
kutibiwa kwa kutumia pamba safi iliyochovywa kwenye dawa aina ya Campho–Phenique, ambayo hupatikana
kwenye maduka ya dawa za mifugo. Matibabu ya muda yanaweza kuliondoa tatizo
hilo.
Uvimbe unaweza kutibiwa kwa namna hiyo
hiyo, lakini lazima uweke matandazo ya kutosha mahali wanapoishi ama uweke ubao
ili wasikanyage kwenye waya wa kwenye kizimba.
Inzi na wadudu wengine warukao
wanawasumbua sungura, na wanaweza kuzuiwa kwa kunyunyizia dawa za kuua wadudu
ambazo zinapatikana kwenye maduka ya mifugo. Usitumie dawa za kupuliza kwa
sababu zina madhara kwa sungura hasa katika mfumo wa upumuaji na zinaweza
kuwaua.
Walishe sungura wako chakula maalumu
kwa wastani wa wakia tatu kwa siku kwa kila mnyama. Wape maji safi na salama ya
kutosha. Nyongeza ya chakula ni nyasi pamoja na majani mabichi au kabichi.
Pendelea vyakula vya nyongeza vya
kijani. Kwa kuwa sungura wanacheua na mara nyingi hula usiku, basi hakikisha
unawalisha vyema nyakati za jioni.
Kila kizimba lazima kiwe na jiwe la
chumvi maalumu kwa sungura, ambalo linapatikana kwenye maduka ya vyakula vya
mifugo. Hili ni muhimu kwa sababu linaongeza madini ya chumvi mwilini. Sungura
daima hulilamba wakati wowote anapotaka. Bila kuweka madini ya kutosha kwenye
milo yao, sungura jike anaweza kuwatafuna watoto wake.
Hakikisha vyombo unavyovitumia
kulishia ni visafi daima, kuanzia vile vya chakula na maji.
...................................................................................................
...................................................................................................
Tags:
SUNGURA
