Sasa


UFUGAJI WA SUNGURA,AINA NA MAGONJWA YAKE I Mshindo Media


Ufugaji Sungura na Magonjwa yake
UFUGAJI WA SUNGURA,AINA NA MAGONJWA YAKE 
Katika makala iliyotangulia tulizungumzia namna ya kutayarisha mabanda na lishe mbalimbali za sungura, katika makala hii tutazungumzia aina na magonjwa mbalimbali ya sungura, endelea…

AINA MBALIMBALI ZA SUNGURA (RABBIT BREEDS):
Kuna aina zaidi ya 45 za sungura duniani kote. Aina maarufu zinazojulikana Afrika ya Mashariki ni hizi zifuauatazo:


1. NEW ZEALAND WHITE :
Sungura hawa ni weupe na rangi ya machoni ni hudhurungi (Pink) iliyokoza karibu na nyekundu. Hubaleghe mapema (miezi sita), huzaa
watoto saba au zaidi na wanaweza kuwanyonyesha vizuri. Nyama yao ni laini na ngozi zao ni nzuri kwa kutengenezea vitu vya mapambo. Wakubwa wanaweza kufikia kilo 2-4.

2. CALIFORNIA WHITE:
 Ni weupe wenye weusi katika ncha za masikio, midomo, pua na mkiani. Wanatoa nyama nyingi (kilo 3.5- 4.5). Vilevile wanabaleghe haraka (miezi 6), wanazaa watoto wengi (7-11) na ni wanyonyeshaji wazuri, ngozi zao vilevile zina thamani kubwa.

3. CHINCHILLA:
Wana mchanganyiko wa manyoya meusi kwa meupe na kuonekana na rangi ya khaki (grey). Thamani ya ngozi yao (pelt) ni kubwa. Wanazaa watoto wachache na huchelewa kubakekhe (miezi 9). Wanafikia uzito wa kil 5-7. Sungura hawa wanapatikana katika rangi mchanganyiko kama rangi ya udongo na zilizofifia kuelekea weusi
CHINCHILLA NA GEMAN GIANT

4. GERMAN GIANT:
 Sungura hawa ni weusi tititi na wana sifa zile za New Zealand White. Aina (kabila) zingine zinazopatikana katika nchi za Afrika ya Mashariki ni Flemish Giant, Angora (huzalisha sufi-fur), Earlop, Dutch, Agout, Chaqured Giant na Frank Vender.

MAGONJWA MAARUFU YA SUNGURA:
Sungura huwa hawapati magonjwa mengi. Hata hivyo wakiwekwa katika mazingira machafu wanaweza kushambuliwa na magonjwa maarufu yafuatayo:

1. COCCIDIOSIS:
Hushambulia sana sungura wadogo. Sungura huharisha (kinyesi cheupe na mara nyingine kilichochanganyika na damu), hukosa hamu ya kula na huonekana wachofu kutokana na kukosa maji mwilini. Ugonjwa huu huzuilika kwa dawa za aina ya coccidiostats ukiwahi mapema. Ukichelewa unaweza kuua sungura ndani ya masaa 48. Ugonjwa huu ni mgumu kutibika, hivyo basi ni muhimu kuuzuia kwa kuweka mazingira waishio sungura katika hali ya usafi kwa kusafisha mabanda kila siku na kuzuia vinyesi kuchanganyika na chakula au maji, lishe bora kutumia dawa za kukinga katika chakula na maji, kuwatenga wanyama walioathirika na ugonjwa huu na banda na vyombo kuoshwa
na disinfenctants kama V-rid. Baadhi ya dawa zitumikazo kutibu ugonjwa huu ni kama vile Amprolium, na za jamii ya salfa kama sulfadiazine,na trimethoprim(trimazine, typhoprim).

  1. PNEUMONIA:
Ni ugonjwa unaoathiri mapafu na njia za pumzi na sungura kuonekana kuvuta hewa kwa shida sana. Macho na midomo huonekana bluu kutokana na kukosa hewa ya oksijeni. Ugonjwa husababishwa na bakteria aina ya Pasteurella multocida au staphylococcus spp ambao husambazwa kwa upepo, vyombo au mikono michafu.
Ugonjwa huu hutibika kwa dawa za kuua bakteria Fluban (enrofloxacin), CTC 20% au Tylosin na nyinginezo.

3. MUCOID ENTEROPATHY/ ENTEROTOXAEMIA:
Ugonjwa huu husababishwa na bakteria wa aina ya Escherichia coli au kukosekana kwa fibre katika lishe ya sungura na husababisha kuharibika kwa njia ya chakula (gut). Dalili kubwa ni pale sungura anapotoa kinyesi kama ute (gelly like) na kuloana sehemu yote ya nyuma. Wanaoathirika zaidi ni sungura wenye umri kati ya wiki 3 hadi 6 na hufa haraka sana wapatapo ugonjwa huu. Utaweza kuwanusuru sungura wako kwa kuwaongezea chakula cha majani kama Lucerne, ukoka na mengineyo.
Vilevile unashauriwa kuwatoa sungura walioathirika katika kitengo (unit) zako za uzalishaji (Breeding units) hali hii ikijitokeza. Ugonjwa huu unaweza kutibika kwa kutumia dawa kwa mfano, Cholestyramine, kumchoma mnyama aliyeathirika sindano za dawa za kuua bakteria zenye wigo mpana wa kufanya kazi kwa mfano dawa ya Doxycol /Cotrimoxazole/OTC 20% vilevile sindano ya vitamini B.

4. EAR CANKER (MANGE):
 Ugonjwa huu husababishwa na viroboto na vijidudu vingine. Hauleti vifo lakini huleta adha kutokana na muwasho unaosababisha vipele na hatimaye sungura kutokwa na damu upande wa ndani wa masikio. Hutibiwa kwa kupulizia Hydrogen peroxide au dawa nyingine yeyote ya vidonda. Vilevile, Unaweza kuondosha vijidudu hivi kwa kupaka mafuta ya mzaituni kwenye sehemu za masikio zilizoshambuliwa, mafuta haya yatalainisha magamba ya ngozi na baadaye yanaweza kusafishwa vizuri na dawa kama vile V-rid, na mnyama achomwe sindano ya Ivomectin mara mbili kwa mwezi ili kuondokana na tatizo hili.
..............................................................................................
Previous Post Next Post