Uzalishaji wa maziwa ni biashara nzuri sana na
ya kuvutia ambayo huwa na faida nyingi na humfanya mfugaji kuridhika hasa kwa
yule anayependa kazi hii. Hata hivyo, ni lazima kuanza kwa kuweka msingi imara
hata kabla ya kufikiria ni aina gani ya mbegu utaichukua kwa ajili ya
kufuga.
Ni vizuri kufahamu kuwa, usimamizi ni moja ya
jambo muhimu sana ambalo likifanyiwa uzembe linaweza hata kumbadilisha ng’ombe
wa maziwa kuwa na uzalishaji duni kama ngo’mbe wa kienyeji. Aina
mbalimbali za ng’ombe wa maziwa huwa na mahitaji tofauti, hivyo kiwango cha
maandalizi yako ni muhimu sana.
Unahitajika kufahamu kuwa,
unalazimika kufikia mahitaji yako kwa ajili ya lishe, si kwenye mahitaji ya
awali tu bali pamoja na mahitaji ya baadaye ya ngo’mbe wako. Suala hili
limefanya wafugaji wengi kushindwa kuendelea kutokana na kuwa hujiingiza katika
shughuli hii bila kuangalia mambo ya msingi yanayotakiwa pamoja na kuweka
mipango thabiti.
Pamoja na kuwa mahitaji yote kwa ajili ya
lishe na mambo mengine yako sawa, ng’ombe wa maziwa ni lazima kuzalisha
kulingana na umbile lake na uwezo wake kamili. Kama utaweza kumudu kufuga
ng’ombe halisi wa maziwa, ni lazima pia utambue kuwa uzalishaji wa juu wa
maziwa uhitaji pia usimamizi wa hali ya juu. Kwa maana hiyo, ni vyema kufuga
ng’ombe wa kiwango cha kawaida (ikiwezekana chotara) ambaye ataendana na uwezo
wako wa kumtunza.
Ni vyema tukaangalia aina mbili za ng’ombe wa
maziwa ambao wana uwezo wa kuzalisha maziwa mengi;
(i)Freshian(Friesian)
Wakati baadhi ya ng’ombe wakiwa na uwezo wa
kuishi kwa muda mrefu, uwezo wa kawaida wa kuishi kwa Freshiani ni miaka sita.
Hata hivyo, aina hii ya ng’ombe ni wazalishaji wazuri wa maziwa ambao huweza
kuzalisha kilogramu 7800 kwa wastani kwa muda wa siku 360 yakiwa na kiwango cha
chini cha mafuta ikilinganishwa na aina nyingine ya ng’ombe.Ng’ombe aina ya freshiani ni
rahisi kumtambua kutokana na kuwa na rangi nyeusi na nyeupe, na ni ng’ombe
wenye uzalishaji bora wa maziwa. Wanyama hawa ni wakubwa na pia wanaweza kuwa
na mabaka meupe na meusi au mekundu na meupe. Ikiwa watalishwa vizuri, freshian
aliyefikia umri wa kukomaa huwa na uzito wa hadi kilogramu 550 na urefu wa
sentimeta 150 kutoka begani. Mtamba huweza kupandwa, akiwa na umri wa miezi
mitano huku akiwa na uzito wa kilogramu 360.
Aidha, aina hii ya ng’ombe huhitaji ulishaji
mkubwa hivyo hushauriwa kwa wafugaji wenye uhakika wa kuwa na lishe bora na ya
kutosha kwa mwaka mzima.
(ii) Ayrshire
Aina hii ng’ombe huwa na miraba ya kahawia na nyeupe karibu sawa na aina nyingine ya ng’ombe ambao huelekea kuwa na rangi ya (Mahogany). Ng’ombe hawa huwa na wastani wa kawaida, na uzito wa kilogramu 540 katika umri wa ukomavu. Aidha, humudu aina yeyote ya ufugaji na si rahisi kupata matatizo yeyote ya miguu.
Ayrshire huweza kufanya vizuri katika malisho ya aina
yeyote tofauti na aina nyingine ya ng’ombe wa maziwa. Kukiwa na usimamizi mzuri
na ulishaji mzuri, wastani wa uzalishaji wa maziwa ni kilogramu 5400 ikiwa na
kiwango cha juu cha mafuta ukilinganisha na Freshian. Aryshire ni aina nzuri
kwa kufuga hasa kutokana na nguvu aliyonayo pamoja na uzalishaji mkubwa wa
maziwa. Ng’ombe wa aina hii, hutambulika kwa kuwa na umbo zuri pamoja na chuchu
zake kuonekana kuwa zenye ubora. Aidha, utungaji wa maziwa yake, umefanya
maziwa yake kuonekana ni mazuri sana katika uzalishaji wa siagi na jibini.
Maziwa ya Ayrshire yanafahamika
kama “maziwa bora ya kunywa” kutokana na uwezo wake wa kuwa na mafuta ya
kutosha na kiasi kikubwa cha protini. Kwa mfugaji anayeanza, aina hii ya
ng’ombe ni nzuri sana kuanza nayo kasha baadaye kuongeza freshiani baada ya
uwezo wako wa kuhudumia kuwa imara. Mifugo ya asili ni ghali sana na ni ngumu
pia kuwapata, hivyo basi, njia rahisi kwa wafugaji wa maziwa wanaoanza ni
kutafuta ng’ombe bora wa kawaida ambao mara nyingi huwa ni chotara, kisha
kuwaboresha kwa kutumia mbinu ya kupandikiza dume bora na mwenye uzalishaji
mkubwa. Na hii huhitaji elimu ya kutosha kuhusu uchaguzi wa madume.
*Muhimu: Wakati wa kununua ng’ombe kwa ajili ya kufuga, ni vyema mfugaji
ukatambua kuwa, wazalishaji wa maziwa mara nyingi hawauzi ng’ombe wao wenye
uzalishaji mzuri, badala yake huuza wale ambao hawazalishi kwa kiwango kizuri,
wale wenye matatizo kama kutokushika mimba, wenye matatizo ya joto na wale
ambao hushambuliwa na magonjwa mara kwa mara. Kwa maana hiyo, pamoja na aina ya
ng’ombe unayehitaji kununua, ni muhimu sana kuwa mwangalifu usije ukanunua
ng’ombe mwenye shida yoyote kwani hapo ndipo mwanzo wa uzalishaji wako kuja
kuwa wa matatizo na kutokufikia lengo.
Banda na nafasi kwa ajili ya ng’ombe wa maziwa
Kabla mfugaji hajafikiria kuhusu makazi ya
ng’ombe wake, ni vyema sana kujiuliza ni kiasi gani cha mifugo utahitaji kuwa
nao baada ya miaka kadhaa hivyo kukuwezesha kutenga nafasi ya kutosha kwa ajili
ya mifugo utakayoleta. Njia rahisi ya kulitambua hilo, ni kujiuliza ni
kiasi gani cha mifugo ungependa kuwa nao baadaye na ni kiwango gani cha
uzalishaji wa maziwa ungetarajia kufikisha kutoka kwa ng’ombe wako.
Swali la kwanza, ni muhimu sana kwa mfugaji
kujiuliza, kwani kiwango cha mifugo hutokana na uwezo wa kiwango cha lishe
utakachohitajika kulisha mara kwa mara. Kwa kawaida, ekari moja ya ardhi
hutoshea kulisha ng’ombe wa maziwa aina ya Freshiani mmoja au Jersey wawili
tu.
Ng’ombe wa maziwa mmoja (Fresian, Guernsey,
Jersey) kiasi cha tani 5 ya lishe ya majani mabichi au majani makavu kwa
mwaka. Hii ni sawa na kilogramu 25,000 za matete au kiasi cha majani
uliyoyaotesha kwenye ekari moja. Pamoja na usimamizi mzuri wa malisho ya nyasi,
au mchanganyiko wa malisho kama mikunde au mimea kama desmodium, ni
dhahiri kuwa bado utahitajika kuwa na angalau ekari ya ziada 0.75 ya eneo ili
kuweza kulisha ng’ombe wako vizuri.
Kwa ujumla, ng’ombe wa maziwa huhitaji lishe
kiwango kikubwa kuliko ng’ombe wa nyama, na mara nyingi huwa na uzalishaji
mkubwa pale ambapo ubora wa lishe ni wa hali ya juu. Hali kadhalika, kama
utazalisha malisho yako mwenyewe, bado utahitaji njia nyingine ya ziada ya
kupata lishe ikiwa itatokea tatizo lolote katika malisho.
Jedwahi hili huonesha kiwango cha lishe
kinachohitajika kwa aina mbalimbali ya ng’ombe wa maziwa, pamoja na ardhi kwa
ajili ya kuzalishia malisho.
........................................................................................................................................................................................................
Ufugaji wa ndani
Katika ufugaji wa ndani, ng’ombe wanahitajika
kuwekwa kwenye hali ya usafi, na makazi yao yawe na ulinzi wa kutosha na yenye
kuwapatia uhuru. Wafugaji walio wengi wamekuwa wakiwekeza fedha nyingi katika
kuwajengea mifugo, na mwishoni kuishia
kukosa fedha kwa ajili ya kulishia mifugo
hiyo. Mfugaji anayeanza, anashauriwa kujengea mifugo yake makazi mazuri na ya
gharama nafuu na baadaye kuendeleza mabanda hayo kutokana na mapato
yanayopatikana.
Mambo ya kuzingatia katika ujenzi wa mabanda
Nafasi: Ng’ombe mkubwa anahitaji kuwa na nafasi ya kutosha kwa ajili ya
chakula, kupumzika pamoja kufanya mazoezi jambo ambalo wafugaji walio wengi
hawazingatii na badala yake huweka mifugo yao katika nafasi ndogo ambayo
mwishoni hudidimiza ukuaji wa mnyama na uzalishaji kwa ujumla. Kwa mantiki
hiyo, ng’ombe mmoja mkubwa anahitaji mita za mraba 8 mbali na eneo lake la
kupumzikia. Njia rahisi ni kutenga eneo hili mbele ya zizi/banda. Kumbuka,
unapokuwa na nafasi kubwa, ndipo unapotengeneza uzalishaji mzuri.
Paa: Ni vyema kukawa na paa kwa ajili ya kuilinda mifugo dhidi ya
upepo, mvua pamoja na jua kali. Hakikisha paa linakuwa juu, ili kuipa uhuru
mifugo yako kutembea ndani ya banda bila tatizo lolote. Hakikisha mteremko wa
paa hauwezi kuathiri sehemu ya mifugo kupumzika na sehemu ya lishe hasa kwa
kuruhusu maji kuingia katika sehemu hizo.
Sakafu: Hakikisha sakafu inakuwa na mfumo mzuri wa mifereji kwa ajili ya
kuruhusu maji na mkojo kupita hivyo kuwaweka mifugo katika hali nzuri. Unaweza
kutengeneza sakafu ya simenti ambayo ni rahisi kusafisha. Hata hivyo kwa kuwa
inagharimu fedha, mfugaji anaeanza, anaweza kutumia udongo wa mfinyanzi au aina
nyingine ya udongo mgumu kutengeneza sakafu. Endapo utasakafu banda, sakafu
isiwe inayoteleza kwa kuwa ng’ombe wanaweza kuteleza na kuumia. Sakafu iwe na
mwinuko kidogo na mwinuko uelekee sehemu ya kutiririshia mkojo na kutolea
kinyesi.
Matandiko: Eneo ambalo mifugo hupumzikia, ni vyema kukawa na matandiko.
Unaweza kutumia malighafi ya aina yeyote kavu ambayo huweza kunyonya mkojo na
samadi. Matandiko hayo ni lazima kubadilishwa mara kwa mara.
Vihondi vya maji na chakula: Hakikisha kuna vihondi vya kutosha kwa ajili
ya chakula na maji. Mabanda ni vyema yakawa karibu na vyanzo vya upatikanaji wa
maji safi na salama. Kwa wastani, ng’ombe mmoja anahitaji kunywa maji kiasi cha
lita kati ya 50 au 80 kwa siku sawa na ndoo 5 hadi 8 za maji (za ujazo wa lita
10).
Shimo la mbolea: Mifugo inayolishwa vizuri hutoa samadi
nyingi hivyo huweza kuwa tatizo kwa watu wanaokuzunguka hasa ikiwa inatapakaa
kila mahali na kusababisha kuwepo kwa harufu mbaya. Kama utafuga mifugo mingi
katika eneo dogo bila kuwa na sehemu maalumu ya kuweka mbolea inayotokana na
mifugo hiyo, basi ni dhahiri kuwa utasababisha kutokuelewana na majirani,
lakini pia kutasababishia wanyama kukaa katika hali ya usumbufu. Ni vyema
kuandaa shimo maalumu kwa ajili ya samadi hasa kwa ufugaji wa ndani, kabla ya
kutumia kwa ajili ya kuweka kwenye mashamba ya malisho.
Namna ya kuanza ufugaji kwa urahisi
Kabla ya kuamua kufanya biashara ya uzalishaji
wa maziwa, maandalizi mazuri ni moja ya sababu itakayokupa mwanga kufanikiwa au
kutokufanikiwa. Hata kabla ya kuwaza nia aina gani ya ng’ombe utanunua, ni
lazima kufikiri kwanza ng’ombe huyo utamlisha nini.
Fikiria lishe, fikiria nyasi
Ili kufuga ng’ombe, ni lazima uwe na lishe ya
kutosha. Huwezi kumuendeleza ng’ombe kuzalisha wakati hauna lishe bora ya
kutosha, ikiwa ni pamoja na nyasi, mikunde na majani ya nafaka. Moja ya njia
nzuri ya kuzingatia ni nyasi. Mfugaji anayeanza, ni lazima kuzingatia haya kwa
ajili ya lishe;
• Hakikisha unatunza nyasi za asili zilizopo
katika shamba lako la malisho
• Ongeza kwa kuotesha majani mengine mapya
katika shamba lako
• Nunua malisho ambapo unaweza kuswaga mifugo
yako kwenda kula
• Kodisha au nunua eneo kwa ajili ya kuotesha
malisho kisha kukata na kupeleka kulishia mifugo
• Nunua majani kutoka kwa watu wanye malisho
au wanaofanya bishara ya kuuza majani yaliyokatwa tayari.
............................................................................................................................................................
............................................................................................................................................................
Tags:
UFUGAJI NG'OMBE